ETETA | Home juu

Habari na Matukio

imewekwa tarehe 2019-10-04

RC SANARE AMPONGEZA DC MOROGORO UJENZI SHULE ZA SEKONDARI MOROGORO,MJIMPYA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro  Mhe. Regina Chonjo kwa Usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Majengo ya Shule za Sekoondari Morogoro na shule ya sekondari Mji Mpya zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mhe. Sanare ametoa pongezi hizo Oktoba 3, mwaka huu alipotembelea Shule ya Sekondari ya Morogoro ambayo iko katika hatua za mwisho za  ukarabati wa majengo yake na shule ya Sekondari ya Mji Mpya ambayo nayo ujenzi wake upo hatua za mwisho baada ya majengo yake ya awali kubomolewa ili kupisha Ujenzi wa mradi wa Reli ya mwendokasi (SGR) .

Akiwa katika shule ya sekondari Morogoro, Mhe. Sanare amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi billioni moja kwa ajili ya ujenzi huo hivyo ilikuwa ni wajibu wake kukagua namna ya fedha za Serikali zilivyyotumika katika ujenzi huo.

“Serikali imeleta hapa kwenye shule hii zaidi ya shilingi billion moja, hivyo ni jukumu letu kukagua namna fedha ya Serikali ilivyotumika, nashukuru Mungu kazi imekwenda vizuri, nichukue nafasi hii kuipongeza kamati ya shule iliyosimamia ujenzi huu lakini pia nikupongeze Mhe.  Mkuu wa Wilaya kwa kazi nzuri ya kusimamia kazi hii,” alisema Sanare.

Aidha, Sanare amemtaka Mkandarasi anaefanya kazi ya ukarabati wa shule hiyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi  katika muda wa siku kumi alizoongezewa kwa kuwa alipaswa kukamilisha ujenzi huo Septemba 26 mwaka huu.

Amesema anaamini ifikapo tarehe 10 Oktoba mwaka huu atakabidhiwa majengo hayo hivyo ni wajibu wao Wakandarasi wa ujenzi miradi hiyo kuhakikisha wanatumia siku zilizobaki kufanyakazi kwa bidii ili kukabidhi majengo hayo.

Sambamba na hayo Mhe. Sanare amewataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii ili kupandisha ufaulu wa shule yao kwa kuwa Serikali imeboresha miundombinu hivyo hakuna sababu ya kutofanya vizuri  kwenye mitihani yao.

Ukarabati wa Shule ya sekondari Morogoro iliyoanzishwa mwaka 1954 umegharimu zaidi ya billion 1.04 ukihusisha  madarasa 29 majengo kwa ajiliya maabara 4, Ofisi za walimu 17, Jiko, mabweni 8, Ukumbi wa Mikutano, Matundu ya vyoo 85, Mabafu 24, Mfumo wa Maji, Mfumo wa Umeme na nyumba za walimu 12.

Akiwa katika shuleya Sekondari ya Mji Mpya alipokea taarifa ya ujenzi kutoka kwa Mkuu wa shule hiyo Zakayo John na kuelezwa kuwa ujenzi huo unapaswa kukamilika  Octoba 25 mwaka huu kwa sasa ujenzi huo umefikia zaidi ya  asilimia 88 jambo ambalo alipongeza kwa kasi  ya ujenzi na kazinzuri iliyofanyika.

Hata hivyo Mhe. Sanare  amemuagiza Mkuu wa Shule hiyo kuishi shuleni hapo  punde tu ujenzi wa nyumba mpya ya walimu utakapokamilika badala ya kuishi mbali ya eneo la shule na vinginevyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo amemshauri Mkuu wa shule ya Mji Mpya kuwa endapo fedha zitabaki kwenye ujenzi wa shule ya mji mpya fedha hizo zitumike kukarabati baadhi ya miundombinu  ya  Shule ya sekondari Tushikamane ambayo walikuwa wakitumia kwa muda kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa shule yao ya Mji Mpya.

Amesema hali si nzuri katika shule hiyo hasa baada ya kutumiwa na wanafunzi wa shule mbili wakati miundombinu yake ilijengwa kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa shule moja pekee.

Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Mji Mpya Umegharimu zaidi ya shilingi billion Moja na nusu ambapo tayari wanafunzi wa shule hiyo wamesharejeshwa katika majengo yao kwa ajili ya kuendelea na masomo wakati baadhi ya majengo yakiendelea kufanyiwa  umaliziaji kwenye baadhi ya maeneo.

 

MWISHO

 

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2019-09-09

Naibu Waziri Zanzibar atembelea Vijana Morogoro

Vijana wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo ili waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira na kujiinua kiuchumi badala ya kusubiri fursa hizo ziwafuate miguuni.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Lulu Msham Abdallah akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro yenye lengo la kuwaona vijana na miradi wanayofanya.

Naibu Waziri Msham amesema ni wakati sasa vijana kubadilika na kuzifuata fursa zilipo badala ya kusubiri ziwafuate wao lengo likiwa ni kujikwamua kiuchumi.

“vijana lazima tubadilike sisi ndio viongozi, ukitazama sasa viongozi wengi wa serikali zetu ni vijana, kwa hiyo tubadilike zinapokuja fursa tujue namna ya kuzifuata tusisubiri zitufuate”, Alisema Naibu Waziri Msham.

Aidha amewataka vijana kufuatilia fursa zilizopo kwa kufika katika Ofisi za Halmashauri ili kuweza kupata fursa zilizopo kwa wakati husika huku akisisitiza kwamba fursa zipo nyngi na fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana nazo  zipo.

Amebainisha kuwa Serikali zote mbili zinajitahidi kuhakikisha vijana wanakuwa na maisha bora kwa kutengeneza fursa mbalimbali kwa vijana hivyo vijana ni wajibu wao kuzifuata fursa hizo pasipo kusubiri ziwafuate.

Katika ziara yake Mhe. Mshamu amesema yapo mambo ambayo anataraji kujifunza kwa vijana wa Tanzania bara ili kuyapeleka kwa upande wa vijana wa Zanzibar na pia yapo mambo ambayo amewaletea vijana wa Tanzania bara kutoka Zanzibar ikiwemo kilimo cha matunda ya Shokishoki ambayo soko lake ni kubwa.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake Naibu waziri Msham ametembelea Mradi wa uzalishaji wa Maziwa uliobuniwa na kikundi cha wanafunzi waliomaliza Chuo Kikuu cha Kilimo cha SUA na baadae kutembelea kikundi cha Kilimo cha Mzinga ambapo ametoa wito kwa vijana hao kuto kata tamaa na kuhakikisha wanazifanya shughuli hizo kwa maslahi mapana.

Ziara ya Naibu Waziri Lulu Msham Abdallah Mkoani Morogoro imeanza jumapili Agost 8 mwaka huu na inataraji kuendelea siku ya jumatatu Agosti 9 mwaka huu kwa kukagua miradi mbalimbali inayoendeshwa na vijana waliojiunga katika vikundi ili kuona namna ambavyo wanaweza kujinasua kutoka katika wimbi la umasikini


Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2019-08-29

Afisa Elimu Mkoa ataka ushirikiano kwa watendaji shule za Sekondari Ifakara, Kilombero.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro Eng. Mwl. Joyce Baravuga amewataka Maafisa Elimu kata na Wilaya ,  wadhibiti Ubora wa shule na wadau katika sekta hiyo kushirikiana ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika shule kwa lengo la kuinua kiwango cha Elimu mkoani humo.

Eng. Mwl. Joyce Baravuga ameyasema hayo Agosti 29, mwaka huu siku  ya kwanza ya ziara yake maalum yenye lengo la kufanya ufuatiliaji wa shule za sekondari ambao utatoa tathmini ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazopelekea kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu katika shule Mkoani Morogoro.


Ushauri huo wa Eng. Mwl. Joyce Baravuga umekuja mara baada ya kufanya ufuatiliaji katika shule mbili za Sekondari za Kilombero na Ifakara zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara na kubaini uwepo wa changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uwepo wa ushirikiano mdogo kuanzia Waratibu Elimu ngazi ya kata hadi Wilaya jambo linalopelekea kutokuwepo kwa kauli moja ya kudhibiti kiwango cha taaluma katika shule zao.


“Niwaombe Ndugu zangu Maafisa Elimu kata na Wilaya mshirikiane kwa pamoja katika kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika shule zetu hizi ili kuwasaidia hawa walimu kuinua kiwango cha ufaulu”,alisisitiza Eng. Mwl. Joyce Baravuga


Katika ziara hiyo maalum,Eng. Mwl. Joyce Baravuga kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Elimu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alitumia vigezo 21 ambavyo kwa pamoja vina lengo la kupima kiwango cha uwajibikaji kwa walimu, wazazi na jamii kwa jumla ili kubaini vikwazo vinavyokwamisha kupanda kwa ufaulu katika shule hizo na kuzitafutia suluhisho.


Akitumia vigezo hivyo wakati wa kufanya ufuatiliaji katika shule ya sekondari Kilombero, Eng. Mwl. Joyce Baravuga alibaini mambo mbalimbali yanayopelekea kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.


Mambo yaliyobainika ni pamoja na kufanya kazi kwa mazoea kwani  baadhi ya walimu walibainika kutojaza baadhi ya taarifa za zamu za kila wiki, kutojaza taarifa za mahudhurio ya walimu na uwepo wa  mikakati dhaifu ya kukabiliana na tatizo la kufanya vibaya kwa wanafunzi.


Kutokana na hali hiyo Eng. Mwl. Joyce Baravugaamemtaka Kaimu Mkuu wa Shule hiyo kuhakikisha anasimamia ipasavyo shughuri za kila siku za kiutendaji na kuwasimamia ipasavyo walimu  wake kutimiza wajibu wao kulingana na miongozo ya Serikali na viongozi wao waandamizi.


Aidha, amewataka Afisa Elimu wa Ifakara mji pamoja na Mratibu Elimu kata kutoa ushirikiano wa kutosha kwake na kwa viongozi wengine wa ngazi ya Mkoa na Wilaya.


Akiwa katika shule ya sekondari Ifakara ambayo imefanya vibaya katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu na kuwa ya mwisho kimkoa, Eng. Mwl. Joyce Baravuga ametoa onyo kwa walimu wa kiume ambao  wanajaribu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike na kusababisha kufanya vibaya kwenye mitihani.


Amesema yeyote atakaebainika kuwa na mahusiano hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria huku akisisitiza kwamba taarifa za vitendo hivyo ameshazipata na anazifanyia kazi.


Kwa upande wake Afisa Taaluma Mkoa wa Morogoro Mpakuli Jackson amewataka walimu wa shule ya Sekondari Ifakara kuwajibika ipasavyo ili kubadili matokeo mabaya ya ya mwaka huu ya kidato cha sita.


Amesema hakuna wa kumtupia lawama isipokuwa wanapaswa kuangalia wapi walipokosea na kurekebisha kasoro hiyo haraka ili kuinua kiwango cha taaluma katika shule zao.


Nao Wakuu wa shule za Sekondari za Ifakara na Kilombero, Maafisa Elimu, pamoja na waratibu Elimu kata  wamepokea maagizo ya Afisa Elimu  Mkoa na kuahidi kuyatekeleza ili kuinua kiwango cha Elimu katika shule zao.


Ziara maalum ya ya Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Mwl. Joyce Baravuga yenye lengo la kufanya ufuatiliaji wa maendeleo ya shule katika Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro imeanza Agosti 29, mwaka huu katika Halmashauri ya Mji Ifakara na itaendelea kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.


Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2019-09-03

Shule za sekondari Dakawa na Kilosa zaagizwa kuanza Ukarabati.


Na. Hamadi Kwembe, Morogoro

Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Mwl.Joyce Baravuga ameuagiza Uongozi wa Shule ya Sekondari ya Dakawa na Sekondari ya Kilosa kuanza kazi ya ukarabati wa majengo ya shule hizo mara moja kwa kuwa fedha za ukarabati huo zilishaingizwa kwenye Akauti ya shule zao.

Eng. Mwl.Joyce Baravugaametoa agizo hilo Agosti 30 mwaka huu alipozitembelea shule hizo ikiwa ni sehemu ya ziara yake yenye lengo la kufanya ufuatiliaji kwa shule za Sekondari ili kuinua kiwango cha ufaulu katika shule hizo.

Akiwa katika shule ya Sekondari Dakawa Eng. Mwl.Joyce Baravuga alishangazwa kuona Uongozi wa shule hiyo haujaanza kutumia fedha shilingi Millioni 336 zilizoingizwa kwenye Akaunti ya shule hiyo tangu Aprili mwaka huu huku akishangazwa na uwepo wa michakato badala ya kuanza ukarabati.

“Fedha imeingizwa tangu tarehe 27 mwezi wa nne tangu kipindi hicho ni michakato tu imekuwa ikiendelea muda unazidi kwenda kazi bado haijaanza kufanyika, wakati lengo la fedha kuingizwa kwenye Akaunti ya shule ilikuwa ni kupunguza mizunguko ili kazi ianze mapema, kwa hili nashindwa kuwaelewa kabisa”, alisema Eng. Mwl.Joyce Baravuga.

Kutokana na hali hiyoEng. Mwl.Joyce Baravugaameagiza ukarabati huo uanze ndani ya kipindi cha wiki moja na kazi hiyo ikamilike kabla au ifikapo Oktoba 30 mwaka huu huku akiahidi kurudi shuleni hapo kukagua utekelezaji wa maagizo yake hususan kuanza kwa ukarabati wa shule hiyo.

Hata hivyo ameipongeza shule hiyo kwa kufanikiwa kuzuia matokeo mabaya hasa katika Daraja la nne na sifuri kwa miaka mitano iliyopita ambapo amesisitiza kujikita katika kuondoa Daraja la tatu na kubaki na Daraja la kwanza na la pili pekee.

Amesema endapo shule hiyo itafanya vizuri hatosita kuiomba Serikali kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule ya wanafunzi wenye vipaji maalum kwa kuwa ni miongoni mwa shule zinazotegemewa nchini.

Akiwa shuleni hapo Eng. Mwl.Joyce Baravuga alifanya kikao na walimu wa shule hiyo na kusikiliza changamoto zao na kuwataka kushirikiana ili kuinua kiwango cha ufaulu  katika shule yao.

Afisa huyo wa Elimu Morogoro aliendelea kusisitiza Maagizo kama hayo hata alipofika shule ya Sekondari Kilosa, hususan agizo la kutaka ukarabati wa majengo ya shule hiyo kuanza mara moja ili kuondoa changamoto ya uchakavu wa majengo yaliyopo katika shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini.

Taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilosa Mbaraka Kupela ilithibitisha kupokea fedha za ukarabati wa shule hiyo kiasi cha shilingi Milioni 700 tangu Juni mwaka huu lakini bado fedha hizo hazijaanza kutumika jambo ambalo Eng. Mwl.Joyce Baravugaameona ni kinyume cha malengo yaliyotarajiwa.

Katika ziara yake kwenye shule zote mbili, Eng. Mwl.Joyce Baravuga ameendelea kusisitiza kutumika vigezo 21 ambavyo Ofisi yake imeviandaa kwa lengo la kila shule kujitathmini na kuboresha hali ya ufaulu ambapo ameahidi kurudi katika shule hizo ili kufuatilia kwa karibu  utekelezaji wa maagizo yake.


Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2019-09-07

Mkurugenzi, Watumishi watakiwa kushirikiana

Na. Hamadi kwembe - Morogoro

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro wametakiwa kushirikiana katika kuinua taaluma sambamba na kuboresha miundombinu ya Elimu katika Halmashauri yao.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ambapo alitembelea shule za Sekondari Njungwa na Nongwe ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Halmashauri zote za Mkoani humo.

Ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kukagua maendeleo ya shule za Sekondari kupitia vigezo 21 vya kutathimini utendaji kazi shuleni ili kwenda sambamba na Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro kutaka kufahamu sakata la kuuzwa bati zilizonunuliwa kwa fedha ya Serikali kwa ajili ya ujenzi  wa madarasa na nyumba za walimu katika Shule hizo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo Agnes Mkandya alikiri kuwepo kwa sakata ambalo lilimfanya kumvua madaraka ya Ukuu wa shule na kuwa mwalimu wa kawaida kwasababu ya kukiuka taratibu za Serikali na matumizi mabaya ya mali za Serikali licha ya kuwa hilo lilifanyika kwa lengo la kulipa madeni yaliyotokana na ujenzi wa shule hiyo.

“nikweli tatizo hilo limetokea ambapo kulikuwepo bati ambazo zilibaki baada ya kukamilika ujenzi wa madarasa matatu na nyumba za walimu katika shule hizi, lakini wakuu wa shule waliuza bati hizo wakidaikulikuwepomadeni ya mafundi waliojenga majengo hayo pasipo kufahamu mali ya  Serikali  huwa haiuzwi”, Alisema Mkandya.

Mhandisi Baravuga pamoja na lengo la kukagua maendeleo ya shule hizo kitaaluma kupitia vigezo 21  alilazimika pia kutatua mgogoro uliopo kati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na Wakuu wa Shule za Sekondari za Nongwe na Njungwa ambao walisimamia Ujenzi uliokuwa unaendelea katika shule zao na kuvuliwa madaraka yao.

Mhandisi Baravuga aliwataka walimu hao sambamba na Mkurugenzi wao ambaye ndiye kiutendaji ni bosi wao kushirikiana na kuhakikisha wanainua kiwango cha taaluma katika shule hiyo na Wilaya yao kwa jumla.

Ziara hiyo ya Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro ni mwendelezo wa ziara zake katika Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro zenye lengo la kukagua maendeleo ya shule na kufikisha vigezo 21 vya kutathmini maendeleo na utendaji kazi shuleni ambapo tayari ameshatembelea Halmashuri za Wilaya za Kilombero na Kilosa.

 

Soma Zaidi

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani

Subscribe Ili Kupata Taarifa Zetu

Tafadhali ingiza barua pepe kisha bonyeza kitufe cha unganisha kupata habari mbalimbali kuhusu ETETA