ETETA | Home juu

Habari na Matukio

imewekwa tarehe 2020-11-24

MOROGORO ILIYOKUWA GHALA LA CHAKULA, SASA NI GHALA LA ELIMU

Safu ya milima ya uluguru na jiografia nzuri ya mkoa wa Morogoro viliufanya mkoa huo kupata mvua za kutosha zinazowezesha shughuli za kilimo kuendelea katika misimu yote ya mwaka. Hali hiyo ilipelekea Mkoa wa Morogoro kujizolea sifa ya kuwa ghala la taifa la chakula huku viwanda vingi vya kuchakata mazao vikijengwa Morogoro.

Lakini vipi kuhusu sekta ya elimu mkoani Morogoro? Watu wa Morogoro wanapenda kilimo kuliko elimu? Ni nani anayeweza kutenganisha kilimo na elimu?

Matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2020 yamerejesha heshima ya Mkoa wa Morogoro iliyokuwa imepotea kwa miaka mingi iliyopita. Katika matokeo hayo, Mkoa wa Morogoro umeweza kuwa miongoni mwa mikoa 10 iliyofanya vizuri zaidi kwa kushika nafasi ya 8 kitaifa huku ikifaulisha kwa asilimia 87.21%.  

Katika kipengere cha Halmashauri 10 zilizoongoza kitaifa, Mkoa wa Morogoro umeweza kuingiza halmashauri yake ya Malinyi ambayo imeshika nafasi ya 9 kitaifa. Haikuishia hapo, Halmashauri nyingine ya Kilosa kutoka Mkoa wa Morogoro imeweza kushika nafasi ya 6 katika Halmashauri 10 zilizoongeza ufaulu kwa miaka 3 mfululizo. Hongereni sana wana Morogoro.

Kama ilivyo kwa uzalishaji wa chakula, Mkoa wa Morogoro unaenda kuwa ghala la elimu kwa kuzalisha wahitimu walio bora kwa maendeleo ya Taifa letu la Tanzania. Na kwa bahati nzuri, wale wale wanaoshiriki kilimo ndio hao hao wadau wa elimu yaani “Kula na kusoma”. Hii ni pamoja na viongozi wa ngazi zote, Walimu, wazazi, na wanafunzi.

Watu wengi wanaweza wakawa wanajiuliza maswali kwamba, nini kimeurejesha Mkoa wa Morogoro kwenye chati ya kumi bora kitaifa? Gazeti na Habari leo la Novemba 23, 2020 limeandika maoni ya wakuu wa mikoa iliyofanya vizuri katika kichwa cha habari kisemacho “Ma-RC ‘wafunguka’ ushindi Darasa la Saba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare ameeleza kuwa, “ufuatiliaji wa karibu wa ufundishaji shuleni, vikao na wakuu wa shule na walimu wakuu wa shule za msingi vimeuwezesha  mkoa huo kushika nafasi ya 8 kitaifa katika matokeo ya darasa la saba”. Mhe. Loata ameongeza kuwa, alijiwekea utaratibu wa kila siku kabla ya kuingia ofisini kupita kwenye shule moja au mbili kuona walimu iwapo wanafika kazini kwa wakati na kuangalia maandalio yao ya kazi kabla hawajaingia darasani.

Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga, alionesha kufurahishwa na matokeo hayo na kumshukuru Mungu aliyewezesha yote hayo. Katika mtandao mmoja wa kijamii, Mhandisi Baravuga aliandika maneno haya;

“Matokeo ya mtihani wa Darasa la saba 2020 Morogoro tumekuwa wa 8 kitaifa baada ya kupata asilimia 87.21%. Ahsanteni sana sana viongozi wote kwani ushirikiano wenu, ndio umefanikisha kutoka asilimia 78% mwaka 2019 na nafasi ya 16 kitaifa na kufikia ufaulu mkubwa unaoonekana mwaka huu.

Hongera sana viongozi wote kwa kupandisha ufaulu. Hongera sana Malinyi kwa kuingia 10 bora kitaifa. Hongera sana Kilosa kwa kupandisha ufaulu kwa miaka 3 mfululizo. Hongera sana walimu wote kwa kazi kubwa mnayoifanya mashuleni”. Hongereni pia wazazi kwa ushirikiano mzuri. Ahsanteni sana”.  Mhandisi Joyce Baravuga.  

Dalili zinaonesha kuwa, huu ni mwanzo tu wa matokeo makubwa yanayotarajiwa kupatikana Mkoani Morogoro hasa katika sekta ya elimu kwa miaka ya hivi karibuni. Yapo mambo mengi sana yaliyofanyika katika sekta hii ambayo yameanza kuleta matokeo chanya. Ikumbukwe kuwa viongozi wengi wa ngazi za juu mkoani Morogoro akiwemo Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro bado ni wapya.

Hii ni sawa na kusema kuwa, mabadiliko ya uongozi mkoani Morogoro, yameanza kuonesha dalili njema katika sekta ya elimu. Ndiyo maana tunasema Morogoro iliyokuwa ghala ya chakula, sasa inaenda kuwa ghala la elimu.

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2020-11-21

SAUTI YA MWALIMU KWA MWANAFUNZI ANAYEJIANDAA KUFANYA MTIHANI WA TAIFA KIDATO CHA NNE 2020

Ni siku mbili tu zimesalia kabla ya mtihani wa Taifa kidato cha nne kuanza hapo jumatatu tarehe 23 Novemba 2020.

Kijana wangu ninaomba kusema nawe maneno machache kabla haujaingia kwenye chumba cha mtihani wako wa kuhitimu elimu ya sekondari. Kabla ya kuja kuongea na wewe, nilikuwa nawaza hali niliyokuwa nayo mimi zamani wakati nikijiandaa na mtihani kama huu ulio mbele yako. Katika kuwaza kwangu sikuishia hapo, pia nimeikumbuka ile taarifa ya habari ya TBC iliyoanza kwa mhitasari kuwa “Baraza la Mitihani la Taifa latangaza matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka uliopita”. Hapo nimeshika kifua nikahamisika kusema na wewe haya machache;

1.      Mtihani ni utaratibu wa kawaida kabisa wa serikali zote katika kuchambua watu/wahitimu wake ili kujua nani mwenye sifa ya kuwa sehemu flani au kufanya kazi fulani. Tukiruhusu kila mtu ajichagulie kazi ya kufanya au sehemu ya kwenda baada ya kuhitimu masomo yake, baadhi ya kazi hazitapata watu; kazi moja itakimbiliwa na watu wengi kuliko inavyohitajika; baadhi ya kazi zitapata watu wasiostahili; na wengine watashindwa kabisa kuchagua kazi ya kufanya.   

 

Hoja yangu hapa ni kwamba, usiuogope mtihani ulio mbele yako. Wewe sio mkosaji na mtihani kama huo haujawahi kuwa miongoni mwa adhabu zitolewazo shuleni. Ni utaratibu wa kawaida kwa nchi zote. Ndiyo maana umeitwa mtihani wa taifa. Wanafunzi wenzako wote wa kidato cha nne Tanzania nzima watakuwa wanafanya mtihani huo huo unaoufanya wewe. Kama ulivyofaulu mtihani wa darasa la nne, la saba na kidato cha pili, amini kuwa utafaulu pia mtihani huu na kuendelea na hatua nyingine inayofuata.

 

2.      Nikikurejesha katika maisha ya Yesu kristo, wakati ule akiteua mitume wake 12 alikuwa anapita na kuchagua mtu kwa kumgusa tu na kumwambia nifuate bila kutoa mtihani. Huo ndio uliokuwa mtihani mgumu zaidi kwakuwa hapakuwa na nafasi ya kujitetea kwa wale ambao wangependa kuchaguliwa lakini hawakupata nafasi ya kuguswa.

 

Wewe una bahati kwakuwa utapewa kijitabu kizima (booklet) cha kujitetea ili uwe miongoni mwa watakaochaguliwa kuendelea mbele. Kama haitoshi, unaweza hata kuomba kijitabu cha ziada kadri ya uwezo wako ili tu kujitetea kiasi cha kutosha. Hakikisha unatulia na kujaza majibu sahihi na kutunza unadhifu wa kijitabu chako cha kujibia. Fuata sheria na maelekezo yote ya mtihani pamoja na wasimamizi wako. Fanya yako na Mungu atafanya yake kukusaidia.

 

3.      Mwisho, ukimaliza mtihani wako usiondoke nyumbani kabla hujaniona tena nikupe maelekezo kuhusu maisha yako baada ya kuhitimu shule. Una miezi mingi ya kukaa nyumbani kusubiri matokeo yako. Kwa yale ambayo mimi kama mwalimu sikuweza kukukufundisha kutokana na sababu mbalimbali, nitakushauri namna utakavyotumia muda wako kuendelea kujifunza ukiwa nyumbani.  

Wazazi wako wanakuombea mema na wanayo shauku kubwa ya kuona unafanikiwa vyema katika mitihani yako. Sote kwa pamoja tunakutakia kila la kheri ili uje kuwa miongoni mwa watakaochaguliwa kuendelea na ngazi zingine za elimu zinazofuata.

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!

 

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2020-10-26

SALAMU ZA POLE

Jina

YESSE KANYUMA.

Cheo:

Mkurugenzi msaidizi wa Maendeleo ya Elimu Msingi

Wizara

Elimu Sayansi na Teknolojia.

Matibabu

Amefariki akiwa kwenye Matibabu Hospital ya Muhimbili -Moi -Dar es Salaam

Mazishi

Kafariki tarehe 23/10/2020

Atazikwa tarehe

26/10/2020

Mahali pa Mazishi

Kijiji cha:

Mwemage  ( Misenyi) Kagera

Poleni saana

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2020-10-05

Tafakari; SIKU YA WALIMU DUNIANI INANIKUMBUSHA WALIMU KAMA WAFUNGWA

(Pichani ni Mwl. Wilson Anatory akifundisha somo la Kompyuta kwa watoto wa darasa la tano katika moja ya shule za Msingi za Manispaa ya Morogoro)

Si vibaya kukumbuka mawazo ya kitoto niliyokuwa nayo. Nilipokuwa mdogo sikuwahi kufikiri kama ualimu ni ajira. Akili yangu ya kitoto ilinifanya niamini kuwa walimu ni watu waliofanya makosa ya jinai katika jamii, na hivyo kuhukumiwa adhabu ya kulea watoto wa wazazi wengine katika maisha yao yote. Yaaani mzazi akitaka kwenda kazini anawapeleka watoto wake wakashinde kwa mwalimu ili akawachukue jioni baada ya kazi.

Nilikuwa nikifanya ulinganifu kati ya maisha ya shule na yale ya nyumbani. Kwa kiasi kikubwa kulikuwa na uhusianao mkubwa wa malezi kati ya nyumbani na shuleni. Nikiwa shuleni au nyumbani niliweza kufundishwa mambo yaleyale kusoma, kuhesabu na kuandika. Kote huko nilihimizwa nidhamu, utii na bidii katika kazi.

Nikifanya kosa nyumbani, wazazi wangu walikuwa wanakasirika sana kiasi cha kuogopesha. Ilifikia hatua hadi nikawa naogopa kurudi nyumbani ninapogundua nimekosea. Hali ilikuwa hivyo hivyo hata kwa walimu wangu shuleni. Kuna wakati baadhi ya wanafunzi waliogopa kurudi shule kwasababu mwalimu fulani amekasirika na anawawinda kwa nguvu zote.

Kama haitoshi, walimu walionesha kukasirika zaidi kuliko hata wazazi wangu pale ninapoenda kinyume na utaratibu. Walikuwa tayari kusahau watoto wao ili kushughulika na watoto wa wazazi wengine.

Hilo lilitosha kuniaminisha kuwa walimu ni watu waliopewa adhabu ya kulea watoto kwa niaba ya wazazi wangu. Nisingeweza kudhani kwamba ualimu ni ajira waliyoomba wao wenyewe ili kulea watoto wa watu wengine.  Niliamini kuwa kile wanachokifanya ni kujihami ili adhabu waliyopewa isije ikaongezeka zaidi.  

Nikitazama hali za maisha yao ilikuwa ni uthibitisho wa mwisho kuwa ualimu ni adhabu iliyotolewa kwa wakosaji ili kulea watoto wa wazazi wengine wasio na makosa. Sikusita kuwafananisha na wafungwa walioko magerezani wanavyoamuka kwenda kusafisha mazingira na mitaro ya jiji wakati watu wengine wakienda kwenye biashara zao shughuli zingine za uzalishaji mali. Jioni wafungwa hurudi mikono mitupu wakati watu wengine wakirudi na mifuko iliyotuna.

Hadi namaliza kidato cha sita sikuwahi kuona kiyoyozi wala kiti cha kuzunguka shuleni. Walimu na wanafunzi walikuwa wanagombania viti na madawati yanayofanana. Walimu walikuwa wanatumia darasa mojawapo kama ofisi yao; nalo halikuwa na rangi wala hadhi ya kuitwa ofisi. Tumetoka mbali sana.

Katika baadhi ya shule, walimu walikuwa wanakosa hata maji ya kunawa mikono kuondoa vumbi la chaki baada ya kufundisha. Walilazimika kuja kunawa maji ya nyumbani yanayopatikana kwa shida. Achilia mbali umeme ambao wengi tulikuwa tunausoma tu vitabuni bila kujua ni kitu gani kinachozungumzwa. Hili si tatizo kwao kwakuwa walikuwa wanatekeleza kazi yao ya kulea watoto wa wazazi wengine walio ‘busy’ katika shughuli za uzalishaji mali.

Mwalimu akienda kazini, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa pesa yake aliyoenda nayo mfukoni kurudi ikiwa imepungua au imeisha kabisa, tofauti na watumishi wengine ambao kuna uwezekano pesa aliyoenda nayo kazini kurudi ikiwa vile vile au imeongezeka zaidi. Ndiyo maana, mwalimu akistaafu kazi alikuwa kama mtu aliyemaliza kifungo chake jera. Alikuwa aidha hana nyumba kabisa au amejenga nyumba isiyo na hadhi kama watumishi wengine wafanyavyo. Elimu za watoto wake ilikuwa ni kama mchezo wa bahati nasibu.

Leo ninapokumbuka akili zangu za kitoto, Walimu wa zamani ninaomba sana mnisamehe kwa fikira hizo zilizoniplekea hadi kuwafananisha na wafungwa walioko gerezani.

Baada ya akili za utoto kunitoka, niligundua kuwa ualimu nao ni ajira rasmi tena yenye umuhimu mkubwa katika jamii. Ni kazi ambayo mtu husomea na kuomba kwa hiari yake mwenyewe. Infact, hata mimi nimeisomea pia. Kazi hii ni ya wito na ndiyo maana walimu wanaifanya kwa moyo sana bila kujali nini wanakipata kutokana na kazi hiyo. Wanaamini kuwa pale jicho la binadamu lisipofika, jicho la Mungu hufika.

Mwalimu ni kioo cha jamii. Kizazi cha kesho kinamtegemea mwalimu wa leo. Kama moja ya maadui wa nchi yetu ni ujinga, basi mwalimu ni silaha muhimu inayotegemewa kuangamiza ujinga katika Taifa. Kwa msingi huo, ipo sababu ya kuadhimisha siku ya Walimu duniani. Tuitumie kutafakari tulipotoka, tulipo na tuendako kama jamii inayomtegemea mwalimu.

Huwa ninaipenda sana kaulimbiu ya shule moja Mkoani Morogoro isemayo kuwa “The foundation of all Education is Love” ikimanisha kuwa “Msingi wa elimu zote ni upendo. Mtu anayekuelimisha anakupenda, vinginevyo angekuacha upotee. Bila upendo huwezi kuwa mwalimu. Utawafundishaje usiowapenda? Utakaaje na watoto wadogo wa watu wengine siku nzima na mwaka mzima kama huwapendi? Hongereni na poleni sana walimu wote mnaoendelea kupambana na ujinga katika nchi hii.  Leo ni siku yenu, muifurahie!

Mwalimu wa kwanza alikuwa ni Yesu Kristo. Mwaasisi wa taifa letu alikuwa ni Mwl. Nyerere. Hata kule Zimbabwe baba wa taifa lao alikuwa Mwl. Robert Mugabe ambaye pia alikuwa nguzo ya Afrika. Hii ni kazi takatifu na ya wito iliyotangulia kabla ya kazi zingine zote. Ni kazi inayozalisha fani zingine zote. Tuitende kwa moyo bila kujali changamoto zinazotukabili. Heshima kazi!

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!  

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Oktoba 05, 2020

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2020-10-04

Tafakari; MAISHA KATIKA DUNIA TATU

Jumatatu, tatu bora, tatu bomba, tatu mzuka, jiti tatu ni baadhi ya maeneo ambayo namba tatu imejizolea umaarufu. Kama haitoshi kuna watu wanaitwa Tatu. Ndio maana Dunia nazo ziko tatu ambazo usipozielewa vizuri utapata taabu sana kuziishi. Uzuri ni kwamba kila mmoja wetu ni lazima aziishi dunia hizo aidha kwa wakati mmoja au kwa nyakati tofauti tofauti. Wengi wetu huziishi kwa mtiririko kuanzia ya kwanza, pili na kumalizia na dunia ya tatu.

1.      Dunia inayotegemea nishati ya jua, nyota na mwezi

Dunia hii huwezi kuinunua wala kuimiliki lakini unaweza kuiona, kuigusa, kuionja au kuinusa. Angalau kila mtu kwa kiasi kikubwa anafahamu masharti ya kuishi dunia hii bila matatizo. Shule, katiba za nchi, NGO na taasisi mbalimbali zinafundisha masharti haya. Ikiwa hadi leo huna kesi ya jinai, na hauishi mafichoni, basi inawezekana umeshafuzu masharti ya kuishi dunia hii.

2.      Dunia inayotegemea nishati ya umeme tu

Dunia hii unaweza kuinunua na kuimiliki. Hii ni dunia inayokuwepo kwa msaada wa nishati ya umeme tu. Ukiondoa umeme dunia hii inatoweka kabisa. Hii ni dunia unayoweza kuiona kwa macho au kuisikia tu lakini huwezi kuigusa, kuinusa wala kuionja. Hii hupatikana kupitia simu zetu, Komputa na vifaa vingine vya teknolojia kwa msaada wa internet.

Maisha yaliyokamilika kabisa yanaendelea ndani ya dunia hii. Maisha haya yametokana na watu waliotoka dunia ya kwanza na kuamua kuhamia dunia ya pili. Dunia hii itakuwezesha kujua mwenzako anachowaza au anachofanya kwa wakati huo huo hata kama yuko nchi nyingine. Viongozi wanaitumia kuhutubia, wasanii kuburudisha, walimu kufundishia, wafanyabiashara kuuza, na wanafunzi kujifunza. Ni dunia unayoweza kutembea nayo mfukoni au kiganjani.

Changamoto kubwa ya dunia hii, inakuwa na taarifa nyingi sana ambazo zinabaki kuwachanganya au kuwapoteza watu badala ya kuwasaidia. Pili, dunia hii inaathiri sana maisha katika dunia ya kwanza. Kuna wengi wameharibikiwa, wamerubuniwa, wamedanganyika, wametapeliwa, wameibiwa, wametekwa na kupotezwa kutokana na kutojua masharti ya kuenenda katika dunia ya pili.

Muhimu zaidi  ni kwamba, nenda dunia ya pili ukiwa tayari umeshaamua nini unachokitafuta pale. Bila hivyo, utapoteza muda na nguvu yako ya kutosha huku ukiambulia patupu. Tumia maisha unayoyaona pale kama hamasa kwako lakini yasikuumize na usiyaamini sana kwakuwa si wakati wote yatakuwa maisha halisi.

 

3.      Dunia isiyotumia nishati ya jua, nyota, mwezi wala umeme

Dunia hii huwezi kuinunua wala kuimiliki. Hii ni dunia ya kufikirika. Ni ulimwengu wa kiroho. Ili ufike huko, ni lazima uachane na dunia zote mbili zilizotangulia. Masharti ya dunia hii hufundishwa katika nyumba za ibada na kwa watumishi wote walioandaliwa kutoa huduma za kiroho. Tarifa nzuri ni kwamba unaweza kutumia dunia ya kwanza na ya pili kujifunza mambo yatakayokuongoza katika njia sahihi kuelekea dunia ya tatu. Dunia hizo hizo mbili usipozitumia kwa makini, ni sababu tosha ya kupotea njia sahihi kuelekea dunia ya tatu.

Ukizielewa dunia zote tatu haikupi tabu; Jitahidi kuzifahamui aina za binadamu katika kila dunia ili ujue namna ya kuishi. Si unajua bora wali-maharage kuliko wali-mwengu?!!

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Soma Zaidi
imewekwa tarehe 2020-10-04

Tafakari; KIONGOZI BORA HUTOKANA NA MFUASI BORA

Zama zile kila kitu kilikuwa tofauti sana. Wakati na baada ya utumwa watu waliendelea kuathiriwa na mfumo mbaya ya kikoloni. Kama ni Kiongozi aliendelea kuenenda kama Nyampara, na kama ni mfuasi anayeongozwa aliendelea kujihisi kama mateka/mtumwa. Mmoja alijiita Meneja (Boss) na mwingine akaitwa mtumishi neno linalotokana na mtumwa. Kwakuwa wote waliamini katika utumwa, mambo yalikuwa shwari na maisha yaliendelea bila shida.

Katika zama za karne ya 21, mambo yamebadilika. Mwelekeo mpya ni kufanya kazi kama timu (Team work) baina ya kiongozi na wafuai wake. Pamoja na kwamba kila taasisi inakuwa na kiongozi Mkuu,  kila mmoja anatakiwa kubadilika kulingana na hali inayoendelea. Wakati fulani awe kama kiongozi na wakati mwingine awe kama mfuasi. Wakati mwingine inatakiwa kusiwe na kiongozi wala mfuasi bali wote walingane/wafanane ili wafanye kazi kama wachezaji wa timu moja. 

Si wakati wote unatakiwa kuwa mwalimu, wakati mwingine jaribu kuwa mwanafunzi. Hii ni kwa sabau hakuna anayejua kila kitu na hakuna asiyejua kila kitu.

Unaposikia kwamba taasisi fulani haina huduma nzuri, haiendelei, inapata hasara, haina wafanyakazi mahiri, haifai nk; inatokana na sababu moja kubwa kwamba wanataasisi wameshindwa kucheza kwenye nafasi zote mbili. Wanalazimisha kuendana na zama ambazo wakati wake umeshapita. Kiongozi analazimisha kuwa kiongozi wakati wote na mfuasi analazimisha kuwa mfuasi wakati wote. Kila upande unaishia kutupia lawama upande mwingine bila kujua mzizi wa tatizo. Matokeo yake kiongozi anakosa wafuasi; wafuasi nao wanakosa kiongozi wa kumfuata.  kila kitu kinakuwa kivyake vyake;  things falls apart

Huwezi kuwa kiongozi mzuri kama si mfuasi mzuri, na huwezi kuwa mfuasi mzuri kama si kiongozi mzuri.

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Soma Zaidi

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani