Tafakari; SIKU YA KIMATAIFA YA UKIMWI DUNIANI
Jana Desemba 01, 2020 ilikuwa siku ya kimataifa ya UKIMWI duniani. Siku hii inatupa nafasi ya kutafakari juu ya janga hili ambalo bado limeigubika dunia huku likiendelea kudhoofisha afya za watu na hata kusitisha maisha yao. Ni ugonjwa ambao bado wanasayansi hawajapata tiba yake. Huwa ninapenda nisikiapo mtu akijisemea “Hata kama sina pesa, nikiwa na afya nzuri ninamshukuru Mungu”.
Angalau sasa kila mtu anaelewa nini maana ya UKIMWI. Hiki ni kifupisho cha ‘Upungufu wa Kinga Mwililini’. Huu ni ugonjwa unaosababisha mwili kukosa uwezo wa kupambana na vimelea vya magonjwa kutokana na kinga yake kushuka. Hivyo mgonjwa anakuwa na hatari ya kushambuliwa na magonjwa mengine hata madogo madogo kwa urahisi.
Jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba takwimu zinaonesha ongezeko la maambukizi mapya ukimwi kwa vijana walio na umri mdogo kati ya miaka 14-25 ambao ndiyo nguvu kazi ya familia na taifa kwa ujumla. Vijana wengi walio katika umri wanakuwa bado ni wanafunzi wa shule au chuo wakijiandaa kuingia katika soko la ajira.
Mtu anapougua ugonjwa wa UKIMWI au hata ugonjwa mwingine utakaomsababishia kushindwa kushiriki vyema shughuli zake binafsi au za kuajiriwa anakuwa katika hatari ya kupoteza kipato chake huku akilazimika kutumia pesa nyingi kwenye matibabu.
Athari kubwa ya kuugua muda mrefu ukiwa hujiwezi, inapelekea ndugu wa karibu yako nao kuacha shughuri zao ili kukuhudumia wewe. Hivyo, unaweza kukuta katika familia moja jumla ya watu watatu au zaidi hawafanyi tena shughuli zao kikamilifu kwasababu ya kumsaidia mgonjwa mmoja asiyejiweza.
Katika hali kama hiyo kama familia ilikuwa maskini itazidi kuwa fukara zaidi kwasababu ya mtu mmoja anayeugua.
Kwa upande mwingine serikali inapata athari kubwa sana kutokana na magonjwa kama haya. Kama ni mwajiriwa anaweza akapunguza kasi ya uwajibikaji na uzalishaji; pia serikali inaweza kukosa mapato ya kodi kama mtu atashindwa kufanya kazi kabisa. Kumbuka serikali ni mimi na wewe, hivyo serikali yenye wagonjwa wengi kama hawa haiwezi kupiga hatua ya kimaendeleo; nayo itakuwa kama iko taabani wodini.
Zaidi ni kwamba serikali inalazimika kutumia gharama kubwa kutoa matibabu ya bure kwa wenye UKIMWI na wakati mwingine dawa hizo zinanunuliwa kwa mikopo inayolipwa na kodi za wananchi wengine. UKIMWI unaepukika kwa kufuata kanuni zinazoelezwa na wataalamu wa afya.
Hebu fikiria; Kama serikali inatakiwa iwatibu bure watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee, kwanini wewe kijana mwenye nguvu usiukimbie UKIMWI ili bajeti iliyopo iwatosheleze makundi hayo mengine tu?
Tafakari, chukua hatua!
Imeandaliwa na;
Mwl. Wilson Anatory
Kilakala Sekondari